Simba SC yatinga fainali Mapinduzi Cup
Klabu ya Simba, imetinga fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup, baada ya kuwaondosha Singida FG kwa kuifunga mikwaju ya penalti 3-2 kwenye mchezo wa nusu fainali uliochezwa Uwanja wa New Amani Complex, visiwani Zanzibar.
Shujaa katika mchezo huo alikuwa ni Kipa wa Simba, Ally Salim ambaye alidaka penalti tatu za Singida FG zilizopigwa na Gadiel Michael, Hamad Wazir na Meddie Kagere.
Kwa upande wa Simba, waliokosa ni nahodha Shomari Kapombe na Saido Ntibanzokiza.
Kwa matokeo hayo Simba, imetinga fainali na sasa itacheza dhidi ya Mlandege Januari 13.
Simba ni mabingwa wa michuano hiyo wa mwaka 2022 huku Mlandege wakiwa ni mabingwa kwa mwaka 2023.
Katika mchezo huo, timu hizo hadi dakika 90 zinakamilika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 1-1.
Singida FG ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao mapema kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao, Mkenya Elvis Rupia.
Hilo lilikuwa ni bao lake la tano kwenye michuano hiyo na kumfanya kuwa kinara huku akimuacha Allasane Diao wa Azam na mabao manne.
Simba ilicharuka kusaka bao la kusawazisha lakini hawakufanikiwa hadi timu hizo zinakwenda mapumziko.
Kipindi cha pili Simba, ilizidisha kasi ya kusaka bao lakini walikuja kufanikiwa katika dakika 6 za ziada kupitia kwa kiungo wao, Fabrice Ngoma ambaye alifunga kutokana na mpira wa kona uliopigwa na Ntibazonkiza.
Katika mchezo huo Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha aliwapa nafasi wachezaji wake wapya Babacar Sarr na Saleh Karabaka.