Beki wa kushoto wa timu ya Yanga SC, Nickson Kibabage, ameibuka shujaa baada ya kufunga bao muhimu kwenye dakika za majeruhi lililoipa ushindi timu yake wa mabao 2-1 dhidi ya Jamus kutoka Sudan Kusini.
Mchezo huo ni wa pili kwa kila timu katika Kundi C la michuano ya Mapinduzi Cup, ulionekana kuwa unakwenda kuwa sare kwa kila timu kuvuna alama moja.
Kibabage amefunga bao hilo akiitumia vyema pasi safi kutoka kwa Zawadi Mauya aliyepiga akiwa katikati ya uwanja na kuwaacha walinzi wa Jamus walidhani ameotea.
Ushindi huo, unawapa alama 6 Yanga na kujihakikishia kutinga robo fainali ya michuano hiyo.
Mbali na Kibabage aliyefunga bao la ushindi lakini Farid Mussa ndiye aliwatanguliza Yanga mapema kwenye kipindi cha kwanza.
Hata hivyo Jamus walisawazisha bao hilo kupitia kwa David Vicent ndani ya kipindi hicho cha kwanza.
Kipindi cha pili licha ya Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kuwaingiza Max Nzengeli na Mahlatse Makudubela 'Skudu' ili kuongeza nguvu lakini bado milango iliendelea kuwa migumu hadi zilipofika sekunde za mwisho wa mchezo huo.
Yanga itakamlisha mechi zao za makundi Alhamisi kwa kucheza na KVZ.